Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, September 3, 2013

Wanafunzi Wauza vyuma chakavu kujisomesha


  • Kwa sababu ya wazazi wengi kutokuwa na mwamko wa elimu, hivyo kushindwa kuwahudumia watoto wao kielimu, wanafunzi wameamua kutafuta njia ya kupata mahitaji ya kielimu kwa kuuza vyuma chakavu wanavyobadilishana na kalamu na madaftari.

Uzoefu unaonyesha Mkoa wa Shinyanga, ni miongoni mwa mikoa iliyo nyuma kimaendeleo nchini.Hata katika sekta ya elimu, mkoa huo una historia isiyovutia. Kwa mfano, mara tatu mfululizo kuanzia mwaka 2009 hadi 2011, mkoa huo ulishika mkia katika matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.

Mwamko mdogo wa elimu walionao wakazi wengi wa mkoa huo, hususan wazazi unatajwa kuwa moja ya mambo yanayochangia Shinyanga kuwa na maendeleo duni katika elimu.
Katika uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na gazeti hili katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo, mwamko mdogo wa elimu unasababisha baadhi ya wazazi kushindwa hata kugharimia mahitaji madogo ya elimu kwa watoto wao.
Mahitaji haya ni pamoja na kuwanunulia madaftari, kalamu na huduma nyingine ndogondogo zilizo chini ya uwezo wa wazazi.
Wanafunzi na mahitaji ya shule
Katika Shule ya Msingi Mwampunga Bule iliyopo Kata ya Mishepo Shinyanga Vijijini, wanafunzi wameamua kutafuta njia mbadala za kuwasaidia kujikimu na mahitaji ya kielimu, baada ya wazazi wao kukwepa jukumu la kuwahudumia.
Kwa sasa wengi wao wanafanya vibarua mashambani, huku wengine wakibuni mradi wa kutafuta vyuma chakavu ambavyo baadaye wanavitumia kubadilishana madaftari na kalamu kutoka kwa mchuuzi mmoja.
Biashara hii ya vyuma kwa vifaa vya elimu, inakumbusha miaka mingi iliyopita katika histora ya mwanadamu, ambapo biashara zilifanywa kupitia ubadilishanaji wa bidhaa. Kiingereza biashara hii ilijulikana kwa jina la Barter Trade.
Wanavyofanya biashara
Ni saa nne asubuhi nafika katika ofisi ya walimu kwa minajili ya kujitambulisha. Wakati nakaribishwa macho yangu yanatuama katika lundo la mifuko kadhaa inayotumika kuhifadhia nafaka. Kimsingi ofisi hiyo ilionekana kama aina fulani ya stoo maalumu kwa kuhifadhia vitu.
Hata hivyo, ukweli unabaki kuwa hiyo ilikuwa ni ofisi ya walimu wa shule ya Mwampunga Bule. Baada ya kuzungumza na Mwalimu wa Taaluma aliyeitwa Malale Mwandu ndipo nilipogundua siri ya vifurushi vile.
Mwalimu huyo alisema, kwa sababu ya wazazi wengi kutokuwa na mwamko wa elimu, hivyo kushindwa kuwahudumia watoto wao kielimu, wanafunzi shuleni hapo wameamua kutafuta njia ya kupata mahitaji muhimu katika elimu kama vile kununua kalamu na madftari.
Alisema mbinu wanayotumia wanafunzi hao ni kutumia muda wao wa ziada wawapo majumbani kutafuta vyuma chakavu, ili kubadilishana na mmoja wa wafanyabiashara anayekuja shuleni hapo mara kwa mara ambaye huwaletea madaftari, kalamu pamoja mikoba ya kubebea madaftari na vitabu.
Anaeleza kuwa waliamua kukubaliana na biashara hiyo baada ya kubaini kuwa hiyo ilikuwa ni njia mbadala ya kuwapatia wanafunzi mahitaji yao. Kwa sababu hiyo, anasema ofisi imekuwa ikitumika kama sehemu salama ya wanafunzi kuhifadhi vifurushi vya vyuma vyao wakisubiri mchuuzi.
“Hapa kwa kweli mwitikio wa elimu kwa wazazi ni mdogo hadi inafikia hatua watoto wanajitafutia mahitaji yao kwa njia hii kama unavyoiona. Na hii inachangia watoto wengine kuacha shule,’’ anasema
Mwalimu huyo anasikitishwa na hali hiyo, kwani pamoja na wazazi kujifanya maskini anasema katika eneo hilo wazazi wengi ni wakulima na wafugaji wazuri tu.
Kwa bahati nzuri siku hiyo ilikuwa ndio siku ya miadi kati ya wanafunzi na mfanyabishara wa vyuma, Nilishuhudia namna biashara hiyo ya aina yake ilivyokuwa ikifanyika, huku wanafunzi wakiwa wamejipanga katika mstari.
Kwa upande wake, mfanyabiashara huyo, Shema Paulo anasema mbali ya kutumia biashara hiyo kujiingizia kipato, anatumia fursa hiyo kama njia ya kuwasaidia watoto hao kupata mahitaji yao.
“Hii biashara yangu ni ya muda mrefu. Kabla sijaamua kuja shuleni hapa nilikuwa nanunua vyuma hivi kwa pesa, lakini kutokana na wenyeji wangu maeneo haya nikawa nakutana na watoto wengi mitaani muda ambao naona ni wa kuwepo shule, nikawahoji wakasema tatizo ni mahitaji ya shule” anasema na kuongeza:
“Baadaye nikajiuliza kwanini nisiwaletee vitu hivyo kwa kubadilishana na vyuma chakavu, ambapo hata hapo awali wanasema walikuwa wakifanya biashara hiyo kwa ajili ya kupata pesa za mahitaji mbalimbali hususani ya nyumbani. Niliongea na walimu wakaniruhusu, ndiyo nikaanza kufanya hii biashara.”
Nao wanafunzi wanasema kuwa biashara hiyo imewakomboa, kwani kuna nyakati walikuwa wanakwenda shule kusikiliza tu walimu bila ya kuwa na vifaa vya kuandikia.
“Sisi wazazi wetu hawatujali, wanasema nyie nendeni tu Serikali itawapa kwani ndiyo kazi yao, ndiyo maana tumeamua kutafuta chuma chakavu ili tuje kupewa madaftari na kalamu. Nafanya hivi kwa sababu napenda elimu, nataka nisome” anasema Daudi Manula anayesoma darasa la tatu.
Naye Faustine Deus, anayesoma darasa la tano anasema kuwa shuleni hapo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa vifaa vya kujifunzia. Hata madawati anasema yamekuwa kero, akitoa mfano wa darasa lake ambalo halina dawati hata moja.
“Hata ukiingia madarasani utajua kuna baadhi ya wazazi wana mwamko wa elimu na wengine hawana, kwani licha ya darasa letu kukosa madawati kabisa, lakini kuna baadhi ya watoto wanakuja shuleni na viti vyao kutoka nyumbani. Hao wazazi wao wanajua umuhimu wa elimu, lakini wengine tunakalia magogo ya miti” anaeleza
Mimi nikitoka shuleni napita barabarani kutafuta machuma ili nije kupata kalamu na madaftari. Nafanya hivyo kwa sababu wazazi wangu ni masikini kwa sababu wameshindwa kuninunulia hata kiti cha kukalia darasani” anaongeza kusema mwanafunzi mwingine anayeitwa Anna Sheka.
Ukitoa mahitaji kwa wanafunzi, hali ya shule hiyo nayo inasikitisha, na kwa hali ilivyo ni muhali kwa wazazi kujitokeza kunusuru hali ya mambo. source; mw'nchi

No comments:

Post a Comment