Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, September 8, 2013

Unaweza kuboresha uwezo wako wa kukumbuka?

WA UFUPI

  • Aliweza kuzikariri sauti zetu wafanyakazi wote. Pia aliweza kuzikariri namba zetu wote na namba za ofisi na watu mbalimbali wa nje ambao tulikuwa tunamwomba atuunganishe tuongee nao.

Je, huwa unashindwa kukumbuka majina ya watu, namba za simu, tarehe za kuzaliwa watoto wako au nduguzo? Je, wakati mwingine unasahau mahali ulipoweka funguo. Kitabu chako cha benki au hata kitambulisho chako? Je, inatokea unasahau kama ulikuwa unapaswa kufanya jambo fulani wakati fulani?
Namkumbuka rafiki yangu tuliyekuwa tukifanya kazi pamoja aliyekuwa msahaulifu sana. Aliweza kuondoka kazini akaenda hadi nyumbani, kisha akakumbuka kuwa ufunguo wa chumba chake ameusahau ofisini. Siku nyingine, asubuhi alipanda basi akaenda hadi kazini na alipofika ndipo alipogundua kuwa ilikuwa siku ya Jumapili. Kila mara alipokwenda benki kwenye ATM alinipigia simu nimkumbushe namba yake ya siri ili aweze kuchukua fedha.
Kituko zaidi kilitokea siku aliyokwenda kwa daktari ili kumwomba amsaidie. Alipofika alimwele,za daktari kuhusu tatizo lake ambaye baada ya kumsikiliza alipigiwa simu akaongea. Mara tu alipomaliza yule daktari akamuuliza “Umekuwa na tatizo hili kwa muda gani?” Rafiki yangu akamuuliza daktari. “Tatizo gani, mbona sikumbuki kama nimekueleza tatizo lolote”. Daktari akabaki ameduwaa asijue la kusema.
Uchunguzi ulidhihirisha kuwa rafiki yangu hakuwa na kichaa wala mtindio wa ubongo. Alikuwa na tatizo la usahaulifu lililokomaa. Hii ni tatizo linalowakabili baadhi ya watu na pengine hata kuwasababishia usumbufu mkubwa katika maisha. Je, wewe una tatizo kama hili au kama huna kuna ndugu au rafiki yako mwenye tatizo la usahaulifu. Kama unalo wewe mwenyewe au jamaa yako usisikitike wala kukata tamaa.
Ni tatizo linaloweza kutatuliwa kwa sababu kila binadamu ana kiungo kimoja cha ajabu kinachoitwa ubongo. Ingawa ni mdogo ukilinganishwa na ukubwa wa mwili wa binadamu na wala hauzidi hata kilo mbili na nusu, una uwezo wa kutunza kumbukumbu nyingi zinazoweza hata kujaza kumbi mbili. Kwa hakika unaweza kutunza kumbukumbu za mambo yote ambayo binadamu anaweza kuyapata katika uhai wake wote. Na bado una uwezo wa kutafuta na kutoa habari yoyote iliyoihifadhi kwa muda wa dakika tu. Uwezo huo wa kutunza na kutumia kumbukumbuku na uzoefu uliohifadhiwa ndiyo uliomwendeleza binadamu kuzidi viumbe wengine wote na kumjengea ustawi na ustaarabu wote alionao hadi leo.
Ubongo ndicho chanzo cha hisia, shauku, hamasa, busara pamoja na mawazo na fikara za binadamu. Bila uwezo huu binadamu siyo chochote. Hebu fikiria mtu anapopata maradhi ya akili akawa kichaa. Mtu anaweza kuwa na umbo zuri na akawa mkamilifu katika kila sifa na hadhi, lakini kama hataweza kuumiliki ubongo wake na kuufanya utawale vitendo na hisia zake, utu wake utakuwa umepungua. Mwenendo wa binadamu hutegemea maarifa na uzoefu wake alioulimbika zamani na ambao anaweza kuutumia kama ulivyo au kuufanyia mabadiliko yanayokidhi haja ya wakati alionao
Kutokana na dhana hii ni dhahiri kuwa uwezo wa kukumbuka kwa binadamu ni muhimu sana. Na hapana shaka kama hana uwezo au uwezo wake ni mdogo anaweza kujifunza kukumbuka masuala au mambo mbalimbali. Anachotakiwa ni kuimarisha msuli mmoja wa akili zake unaoweza kumjengea uwezo wa kuhifadhi kichwani, akilini au moyoni kama watu wengine walivyozoea kusema.
Wengi wetu tuliosoma zamani kabla ya uvumbuzi wa vikokotozi, tulijifunza na kukariri orodha za hesabu za kuzidisha tulizozoea kuziita ‘table’ orodha ya 2 iliyoanzia kwenye 2 x 1 hadi 2x12 mpaka orodha ya 12 iliyoanzia 12 x 1 hadi 12x12. Pia tulijifunza na kuweka kichwani fomula mbalimbali. huu ni mfano mdogo tu wa kuonyesha jinsi tulivyoweza kujifunza kukumbuka.
Siku zote ninapoandika kuhusu uwezo wa binadamu huwa nakumbuka kisa cha msichana niliyefanya naye kazi ofisi moja zamani. Yeye alikuwa na ulemavu wa kutoona.
Aliajiriwa kuhudumia mtambo wa kutawanya mawasiliano ya simu “telephone exchange” mtambo huo ulikuwa umeunganishwa kwenye simu za mezani za vyumba vyote vya ofisi.
Msichana alikuwa anapokea simu zote kutoka nje na kuzielekeza kwa wanaohusika. Pia sisi wafanyakazi wote tulikuwa tukiwasiliana naye kumwomba apige simu sehemu mbalimbali ili tuongee na watu tuliowataka. Kwa kuwa alikuwa haoni hakuna hata mmoja wetu aliyeamini kuwa angeweza. Lakini baada ya kuelekezwa kwa siku chache tu aliimudu kazi yake.
Aliweza kuzikariri sauti zetu wafanyakazi wote. Pia aliweza kuzikariri namba zetu wote na namba za ofisi na watu mbalimbali wa nje ambao tulikuwa tunamwomba atuunganishe tuongee nao. Licha ya kuzifahamu namba zote hizo aliweza kuzipiga kwa kuzungusha kigurudumu cha mtambo wa simu kilichokuwa na namba 0 – 9. Licha ya kigurudumu hicho, mtambo wenyewe ulikuwa na vitu vingi vya kubofya ili kuruhusu simu kutoka ndani kwenda nje na za ndani kutoka nje. Jambo la kushangaza zaidi aliweza kutambua namba za simu na majina ya maofisa mbalimbali tuliokuwa tunaongea nao.
Kwa mfano kama alipoombwa kuzungumza na Halimashauri ya Jiji, Tanesco, TRA au wizara yoyote alipiga mojamoja bila kuuliza namba. Kama ulitaka kuongea na ofisi au ofisa yeyote kwa mara ya kwanza, alihitaji umtajie namba mara moja au mara mbili. Baada ya hapo usingehitaji tena kumtajia namba hiyo.
Kisa hichi kinatuonyesha maajabu ya jinsi ubongo wa binadamu unavyoweza kufanya kazi. Kama angekuwa hana ulemavu wa kuona angeandika orodha ya majina ya watu, asasi na namba za simu. Au labda angekuwa na orodha walau iliyoandikwa kwa maandishi ya wasioona, lakini hakuwa na chochote alichoandika isipokuwa kichwa chake.
Itaendelea wiki ijayo...

Pengine mtu angeweza kufikiria kuwa huu siyo mfano mzuri kwa sababu huyu msichana alikuwa mlemavu. Lakini kuna watu wengine wasio walemavu walioweza kuonyesha uwezo mkubwa wa kukumbuka; Kama yule mtangazaji wa vipindi vya televisheni aliyeweza kutambua majina ya hadi watu 500. Ama Yule aliyefundisha akili yake hadi akaweza kukariri gazeti la kurasa hadi 30. Baada ya saa chache aliweza kueleza habari ukurasa hadi ukurasa na hata kutaja kila ukurasa wenye tangazo na kueleza kila tangazo linahusu jambo gani.
Wakati tunastaajabu uwezo wa watu wengine, ni vyema uelewe kuwa wewe pia unaweza kuboresha uwezo wako wa kukumbuka. Ingawa huwezi kuwa bingwa kama wale tuliwataja, unaweza kuimarisha uwezo wako hadi kufikia kiwango unachokihitaji katika maisha yako ya kila siku.

Zifuatazo ni baadhi ya mbinu ambazo wanasaikolojia wanaamini ukizitumia zitaweza kukusaidia kuimarisha uwezo wako:
1.Kuunda picha katika akili au wazo linalokumbukika.
Unapotaka kukumbuka jambo au tukio fulani inabidi ulihusanishe na picha au wazo utakaloweza kulikumbuka kwa urahisi. Wanamazingaombwe wanapokuwa katika ukumbi huweza kukumbuka hadi vitu 20 vinavyoweza kutajwa bila mpango wowote na watazamaji wake wakati mtu mwingine hawezi kukumbuka kwa urahi hata vitu sita.
Huwa anaweza kufanya hivyo kwa kutumia mbinu maalumu.
Huanza kwa kuwaomba watazamaji wataje vitu vyovyote wanavyopenda. Wa kwanza anaweza kutaja saa, wa pili akataja simu, wa tatu akataja kitambaa cha mkononi na wengine wakaendelea kutaja vitu kadhaa wa kadha. ili kuweza kukumbuka mwanamazingaombwe huwa anahusianisha namba, kitu kilichotajwa na aliyekitaja. Kwa mfano wa kwanza aliyetaja kitu alikuwa mwanamke mnene, hivyo mwanamazingiaombwe atahusianisha saa na namba moja na mwanamke mnene.
Wa pili aliyetaja simu ni mvulana aliyevaa miwani. Hivyo, atahusianisha simu na namba mbili na mvulana mwenye miwani. Wa tatu aliyetaja pete ni msichana mwembamba aliyevaa kitambaa kichwani. Hivyo, atahusianisha pete na namba tatu na msichana mwenye kitambaa kichwani. Wa nne aliyetaja kitambaa cha mkononi ni mzee mwenye kipara. Hivyo atahusianisha kitabaa cha mkononi na namba nne na mzee mwenye kipara.
Katika mbinu hii kumbukumbu zimejengwa kwa kubuni mawazo yanayoweza kukukumbukika kwa kuyahusianisha na vitu vinavyotarajiwa kukumbukwa. Lakini je, tunawezaje kutumia mbinu hii katika maisha ya kila siku?
Kabla hatujatafakari jinsi tunavyoweza kutumia mbinu hii ni vyema tukumbuke kuwa, kwa hakika huwa hatusahau mahali tulipoweka kitu fulani ila kuwa tunapata shida kukumbuka. Hii ni kwa sababu sisi wenyewe hatujiwekei tangu mwanzo mazingira yatayotusaidia kukumbuka.
Tunakumbuka zamani wazee walikuwa hawapeleki fedha benki. Walikuwa wanaziweka katika mtungi au kikasha na kukichimbia ardhini. Lakini walikuwa wakiweka mazingira ya kuwakumbusha mahali walipofukia mali hiyo ili siku watakapokuja kuzishukua wapakumbuke mahali hapo.
Japo hatuwezi kuchimbia hata tunapoweka ufunguo, hatuna budi kubuni picha au wazo litakalitufanya tukumbuke. Kwa mfano tukiweka ufunguo juu ya video baada ya muda inawezekana tusikumbuke kabisa. Lakini kwa mfano kama tukibuni wazo au picha ya kukumbukia hatutasahau. Wazo linaweza kuwa tumeutumbukiza ufunguo kwenye sehemu ya video tunakoweka mikanda. Picha hiyo ya kufikirisha tu itakuwa imara katika kumbukumbu yako na utakapotaka kuuchukua ufunguo, wazo la kuwa umeutumbukiza katika video litakufanya moja kwa moja uende kwenye video.
Kuna mawazo mengine kama vile mti ulioota kwenye paa la nyumba na umeotesha kwenye tawi bahasha na kalenda. Hili linaweza kuwa wazo la kukukumbusha kuwa wazazi wako walio kijijini wamekuandikia barua kuwa nyumba imeangukiwa mti na kuharibu paa na kwamba mwisho wa mwezi uwatumie pesa ili walirekebishe paa.
Ukiunda picha hii itakuwa inakujia katika akili kila wakati wala hutasahau tatizo hilo linalowakabili wazee kijijini. Pia unaweza kubuni wazo la mwanasesere mwenye namba 21 kifuani aliyevaa hereni au mkufu ili kukukumbusha kuwa binti yako anafikisha miaka 21 na unatarajia kumnunulia seti ya mkufu siku ya sherehe yake ya kuzaliwa.
Vile vile inawezekana kutokea kuwa jioni unaporudi kutoka kazini unatakiwa ununue balbu ya taa iliyoungua, kupitia suti yako kwa dobi na kununua karatasi za kuandikia barua. Unaweza kubuni picha inayoonyesha taa inaning’inia kwenye mkoba wako na umevaa karati kyeupe mwili mzima badala ya suti. Picha hii inaweza kabisa kukukumbusha usisahau vitu vinavyotakiwa uhakikishe unakuwa navyo unaporudi nyumbani kutoka kazini.
Kuna mifano mingi ya namna hii itakayokusaidia kuimarisha kumbukumbu zako. Unachohitaji sio kujaribu kukumbuka bali kutafuta mawazo yanayokumbukika.
2. Kutumia neno au vifungu vya maneno
Hakuna vitu ambavyo watu hupaswa kuvikariri na kuvikumbuka kama vile mashairi, nyimbo, tenzi, methali na vitendawili. Kwa mfano, walimu wanapowafundisha watoto alfabeti huwa wanatumia wimbo a b c d e f g; h I j k l m n o p; q r s t …….; Wanafunzi wanapoziimba herufi hizi huweza kupata kumbukumbu ya kudumu ya alfabeti. Vile vile kuna vifupisho wanavyofundishwa kuvikariri kama vile neno APJUSENO linalowakilisha majina ya miezi 4 katika mwaka yenye siku 30 yaani April, Juni, Septemba na Novemba.
Mbinu ya kuunda vifupisho huweza kutumika ili kumkumbusha mtu mambo anayotakiwa kuyafanya wakati fulani au hatua za kutenda kazi au shughuli fulani. Mimi nina rafiki yangu ambaye amebuni neno linalomkumbusha malipo anayotakiwa kuyafanya kila mwezi, Neno hilo ni PAMAULITA ambalo linawakilisha; PA: Pango la Nyumba, MA: inawakilisha malipo ya bili ya Maji; ULI inawakilisha malipo ya Ulinzi na TA: malipo kwa ajili ya Uzoaji wa taka.
3. Kutumia namba zenye kumbukumbu maalumu
Kuna namba ambazo kila mtu anapozisikia humpatia kumbukumbu maalumu. Namba hizo ni kama vile 999 ambayo kwa miaka mingi imehusishwa na kupiga simu kuomba msaada wa polisi au huduma ya zimamoto. Namba nyingine maarufu sana ni kama vile 77 au 88. Pia kuna tarehe zilizo maarufu sana kama 1 Mei, 25 Desemba na nyinginezo. Vile vile, kwa siku hizi tulio wengi tunazijua tarehe zetu za kuzaliwa.

Tunapochagua namba za simu au za siri tunaweza kuchagua ambazo ni rahisi kuzikumbuka kutokana na kuzifahamu na uzoefu zetu. Kuna rafiki yangu ambaye namba yake ya simu ni mwezi na mwaka aliozaliwa.
source;mw'nchi

No comments:

Post a Comment