KWA UFUPI
- Kuna jeshi la Wachina linakuja, wako wengi. Kwenye moja ya picha za magazetini alipata kuonyesha Rais wetu akiwa amezungukwa na Wachina pale Ikulu.
Nitaanza kwa kukumbushia alichowahi kutamka Askofu Desmond Tutu. Aliyasema haya;“ Kuna tofauti ya kimsingi kati ya kuwa huru na kuwa katika hali ya kukandamizwa. Kuwa huru ni pamoja na kupata huduma za msingi za kijamii; kuwa na ajira, maji ya bomba, umeme, makazi bora na huduma za msingi za afya. Kuna maana gani basi ya kuwa huru wakati ubora wa maisha ya watu haujaimarishwa? Kama sivyo, hata kura nazo hazina maana yoyote!” – Desmond Tutu ( William Gumede; Thabo Mbeki And The Battle For The Soul Of The ANC, Uk. 67)
Na mwanafasihi Mtanzania Profesa Kezilahabi anayasema haya: “ Siku hiyo ikifika, utaona ishara itakayokuongoza. Utakapofika pale ambapo kila binadamu lazima afike utajua hukukosea; kwani njia ya kwenda huko inajulikana kwa wote na inakwenda moja kwa moja bila kupinda.
Huna haja ya kusoma kitabu chochote kupata maelezo ya kwenda huko wala hakuna haja ya kusikiliza mahubiri. Hakuna utaalamu unaohitajika , maana utajikuta umefika. Utakapofika utamkuta amekaa peke yake akiwatazama wale wengine . Hao wengine utawatambua maana ni ndugu zako wote.
Wengi kati yao ndiyo wale waliokuwa askari wa mwanga. Wale ambao hutaweza kuwatambua hata kutambulishwa kwao, na wewe utachukua nafasi yako. Usishtuke utakaposikia majina yao; maana, wengi kati yao wana majina makubwa. Utawakuta wanafanya jambo fulani. Wewe pia fanya kama wao bila kuuliza , bila manung’uniko na usikate tamaa. Kwa sasa subiri ishara” ( E. Kezilahabi, Nagona)
Ndugu zangu,
Kuna jeshi la Wachina linakuja, wako wengi. Kwenye moja ya picha za magazetini alipata kuonyesha Rais wetu akiwa amezungukwa na Wachina pale Ikulu.
Rais alivalia ‘ Kijamaa’, lakini Wachina walivalia ‘ Kibepari’- suti na tai.
Naam, China ni taifa kubwa kiuchumi. Uchumi wake unakua kwa kasi kubwa, ni uchumi wa Kibepari.
Na idadi ya Wachina nayo ni kubwa.
Ili kuweza kushindana kibiashara, China kwa sasa inahitaji malighafi nyingi kwa viwanda vyake. China inahitaji nishati pia; mafuta na gesi.
Wachina wameigeukia Afrika. Wachina leo, kwa kutumia uhusiano mzuri na wa kirafiki wa kihistoria, wa tangu wa enzi za Vita Baridi ya Dunia, wanajipenyeza kila kwenye uwezekano wa kuvuna malighafi ikiwamo mafuta na gesi.
Nao wanakuja na ahadi za misaada ikiwamo kutujengea Waafrika barabara, viwanja vya michezo vya kisasa na hata kumbi za kimataifa za mikutano.
Duniani hakuna cha bure. Wachina wanavuna zaidi ya wanachotupa.
Tujiulize; tunataka nini? Tuangalie pia, masharti ya misaada ya Wachina. Tuangalie vilevile mazingira ya ajira wanazokuja nazo Wachina katika kuwekeza kwao hapa kwetu.
Ilivyo sasa, inatokea wawekezaji wa Kichina wanakuja nchini wakiwa na wafanyakazi wao, na wakati mwingine, hata vibarua wa kubeba zege wanatoka China. Hali hii haisaidii kutatua tatizo la ajira kwa vijana wetu.
Hata inapotokea Wachina wakatoa ajira, basi, mazingira ya ajira huwa magumu kwa vijana wetu. Ujira ni mdogo na masharti ya kazi kwa vijana wetu huwa magumu sana.
Tujiulize pia, uwekezaji wa Wachina unatoa fursa kwa Watanzania kupata maarifa ya kiufundi na kiutawala kwenye sekta ambazo Wachina hao wanawekeza hapa nchini?
Hofu yetu, kama nchi, ni kuendelea kuwa tegemezi, maskini, huku nchi yetu ikiwa na rasilimali nyingi.
Tujifunze kwa wenzetu Wahindi nao walikuwa taifa maskini kama sisi. Lakini, waliwekeza zaidi kwenye elimu ya watu wao na kwa lugha yao, Kihindi. Na hata kwenye uwekezaji, wamekuwa wakizingatia zaidi maslahi ya muda mrefu ya India.
Hivyo, na tujitahadhari, na ‘Uvamizi wa Wachina.’ Yumkini umetukuta tukiwa hatujajiandaa, kama taifa. Nimechokoza mjadala. source Mw'nchi
No comments:
Post a Comment