Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Saturday, September 28, 2013

Mali ya bilioni tisa yauzwa kwa milioni 243/-

Makao Makuu Consolidated Holding Corporation (CHC)
UTATA umegubika uuzwaji wa iliyokuwa bohari ya serikali ya Chang’ombe, Dar es Salaam inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh bilioni tisa lakini ikiwa imeuzwa kwa thamani ya Sh milioni 243 tu, Raia Mwema, limebaini.
Hata hivyo, wakati nyaraka za gazeti hili zikionyesha mauzo ya Sh. milioni 243, mrithi wa PSRC iliyokuwa ikisimamia mali hizo na nyingine za serikali chini ya mchakato wa ubinafsishaji, Consolidated Holding Corporation (CHC) taarifa zake rasmi zinaeleza bohari hiyo imeuzwa kwa Sh. milioni 195.9.


Bohari hiyo ilikuwa mali ya lililokuwa shirika la serikali la Biashara Consumer Services lakini lilipobinafsishwa ikauzwa kwa kampuni inayofahamika kwa jina la BCS (2000) na ingawa bohari hiyo haikuwapo katika orodha ya awali ya mali zilizouzwa, Raia Mwema limeelezwa iliuzwa baadaye katika mazingira yenye utata.
Serikali iliuza bohari hiyo kupitia iliyokuwa Tume ya Rais ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma (PSRC) Januari 6, 2005 kwa thamani ya Sh milioni 487.7
Kiasi hicho cha fedha kilikuwa kwa ajili ya BCS kupewa mali zifuatazo za kampuni hiyo ya serikali; jengo la kampuni hiyo lililokuwa katika eneo la Kurasini, magari matano yakiwamo lori aina ya Scania, Fork Lift, Pajero, Canter na gari jingine ambalo aina yake haikutajwa kwenye mkataba wa ubinafsishaji huo ingawa iliandikwa tu namba SU 31639.
Mkataba wa mauziano baina ya kampuni hizo mbili unaonyesha kwamba BCS walitakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha kwa mikupuo minne katika kipindi cha miezi 24.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mkataba huo, wanunuzi wa Biashara Consumers walitakiwa kulipa kiasi cha Sh milioni 37 tu kama malipo ya awali na kiasi kilichobaki cha Sh milioni 449.9 kilipwe kwa mikupuo minne katika kipindi cha miaka hiyo miwili (miezi 24).
Utata unaogubika uuzwaji huo wa bohari hiyo unatokana na ukweli kwamba hakuna taarifa zozote zinazoeleza ni lini hasa uuzwaji wa bohari hiyo ulifanyika na kwa kiasi gani.
Isipokuwa, kinachofahamika ni kwamba Desemba 31, mwaka 2007, Meneja Mkuu wa BCS, Samwel Dyelu, aliandika barua kwa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wake akiomba kuuziwa bohari hiyo.
Katika barua hiyo ambayo haikuwa na kumbukumbu namba na iliyopitia kwa mtu aliyefahamika kwa jina la David Tenga anayetajwa kuwa mmoja wa wanasheria wa PSRC, Dyelu aliomba wapewe hati ya bohari hiyo.
Kichwa cha barua hiyo ya Dyelu kilizungumzia ombi la kuuziwa bohari lakini ndani ya barua yenyewe, ambayo gazeti hili lina nakala yake, maelezo yanaeleza BCS kutaka kupewa hati.
“Kutokana na kulipa Sh. milioni 234 kupitia cheki namba 506384 ya benki ya CRDB, ikiwa ni kutimiza maagizo mliyotupa, kwa heshima na taadhima, tunaomba tupatiwe hati ya bohari ya Chang’ombe.
“Tunahitaji hati hii kwa ajili ya kuombea mkopo kupitia benki ya Azania Bancorp Ltd,” inasema sehemu ya barua hiyo.
Wakati barua hiyo ikiwa imeandikwa Desemba 31, uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kwamba siku hiyo ndiyo ambayo PSRC ilikuwa inatakiwa kumaliza rasmi shughuli zake.
Ingawa hiyo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya kisheria kwa PSRC kufanya shughuli zake, kimsingi ilikuwa imepoteza nguvu tangu Novemba mwaka huu kupitia Sheria ya Bunge namba 26 ya mwaka 2007 ambayo iliondoa shughuli zote za PSRC kwenda Shirika Hodhi la Mali za Umma (CHC).
Katika mahojiano na gazeti hili wiki hii, Tenga alipoulizwa kuhusu masuala ya uuzwaji wa bohari hiyo alisema yalifanyika muda mrefu na hawezi kukumbuka kila kitu kwa wakati huu.
“Ni vizuri ukaenda CHC maana wale wana faili la BCS na Biashara Consumers. Mimi kuna mambo nimeyasahau lakini ukienda pale utakuta kila kitu vizuri kabisa,” alisema Tenga.
Akizungumza na gazeti hili, Dyelu alisema waliuziwa kihalali bohari hiyo ya Chang’ombe kwa vile bohari waliyouziwa kisheria na PSRC ilikuwa na matatizo ya kibenki na hivyo ikauzwa na ndiyo wao wakapewa nyingine.
Ni kweli katika mkataba wa awali, hakukuwepo na bohari ya Chang’ombe.
Lakini tulibaini baadaye kwamba wamiliki wa awali wa Biashara Consumers walichukua mkopo benki na walitumia bohari ya Kurasini tuliyouziwa sisi kama dhamana.
“Hivyo ulifanyika uamuzi wa busara wa kutuuzia sisi hiyo bohari ya Chang’ombe ili kufidia upotevu wa bohari ya kwanza ya Kurasini. Taarifa hizi zitakuwapo tu pale CHC,” alisema.
Alipoulizwa ni kwa vipi waliandika barua katika wakati ambapo PSRC haikuwa na nguvu ya kisheria kufanya kazi hiyo, Dyelu hakutaka kuongea chochote.
Ofisa Uhusiano Mkuu wa CHC, Joseph Mapunda, aliliambia gazeti hili Jumanne wiki hii, kwamba ni kweli BCS waliuziwa kisheria bohari hiyo ya Chang’ombe.
Raia Mwema limeambiwa na vyanzo vyake vya kuaminika ndani ya iliyokuwa PSRC kwamba mmoja wa waliokuwa wamiliki wa BCS ni hayati Salome Mbatia ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ubinafishaji lakini alifariki dunia mwezi mmoja kabla Dyelu hajaandika barua kwenda PSRC kuomba hati ya bohari.
Raia mwema

No comments:

Post a Comment