Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, September 15, 2013

AIBU :Dk. Mwakyembe aibua wizi mpya bandarini



WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam kuvunja mara moja mkataba na Kampuni ya Ulinzi ambayo ilipewa zabuni ya kulinda bandarini hapo, baada ya kubainika kwamba baadhi ya walinzi wa Kampuni hiyo wanajihusisha na wizi wa mafuta katika boya la kupakulia mafuta lililoko baharini.

Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam jana, katika mkutano wake na wafanyakazi wa Bandari, ambapo alisema wamegundua mtindo mpya wa kuiba mafuta unaofanywa na raia mmoja wa kigeni ambaye anashirikiana na walinzi wa Kampuni iliyoingia mkataba na Bandari ya Dar es Salaam.
Alisema hivi karibuni waliwabaini watu waliokuwa wanafanya kitendo hicho na walipogundua wameonwa walifanikiwa kutoroka na kuacha silaha zao katika eneo la tukio.

Mwakyembe aliwataja waliotoroka kuwa ni pamoja na walinzi waliokuwa zamu siku ya tukio, hivyo akaagiza kwamba ifikapo Jumatatu (kesho), picha za walinzi hao zifikishwe ofsini kwake mara moja kwa lengo ya kuzisambaza katika vyombo vya habari.

“Inasikitisha, mradi wa boya hili la mafuta ambalo limejengwa baharini kwa ajili ya kupakua mafuta kutoka kwenye meli kubwa, umegharimu dola milioni 60, halafu leo watu wanakwenda kutoboa na kuiba mafuta... Mwambieni huyo mzungu na watu wake tunawatafuta, haitojalisha ni kigogo yupi yupo nyuma yake, lazima tuwakamate.

“Hawa wahalifu wamekuwa wakizamia baharini na wanatumia maputo yenye uwezo wa kubeba lita elfu 16 hadi 20 kunyonya mafuta katika boya hilo, hii kazi haifanywi na wavuvi bali inafanywa na wataalamu wenye uzoefu na ubaharia,” alisema Dk. Mwakyembe.

Katika hatua nyingine, Dk. Mwakyembe alisema mpasuko unaoendelea katika bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Bandari, unatokana na ulafi wa fedha.

Alisema kabla hajafikiri kuivunja bodi hiyo, mwakilishi mmoja wa wafanyakazi wa Bandari ya Dar es Salaam, anapaswa kuteuliwa haraka iwezekanavyo ili ajumuishwe kwenye vikao vyote vya bodi hiyo.

“Ulaji ndio sababu kuu inayosababisha mpasuko katika Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Bandari, sitosita kuchukua hatua zaidi juu ya mgogoro huu,” alisema Dk. Mwakyembe.

Mwakyembe pia alipongeza juhudi zinazofanywa na uongozi wa Mamlaka ya Bandari, kwa kufanikiwa kupunguza udokozi wa mizigo inayoshushwa bandarini hapo.

Source:Mtanzania

No comments:

Post a Comment