Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Thursday, September 12, 2013

Serikali yatangaza ajira mpya kwa walimu...!!!


SERIKALI imetangaza mpango mpya wa ajira za walimu 28,638 wa shule za msingi na sekondari, katika mikoa inayokabiliwa na changamoto ya uhaba wa walimu.

Mpango huo ulitangazwa juzi na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, wakati akizungumza katika mahafali ya nne ya Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa (MUCE) mkoani Iringa.

Akizungumzia mpango huo, Mulugo alisema walimu watakaomaliza masomo yao awamu hii, wataajiriwa katika maeneo ya vijijini na si katika shule zilizopo mijini kama ilivyozoeleka.

“Tutawaajiri wote hapa hapa, lakini safari hii, hakuna ajira mijini na wote mtakaoajiriwa, tunawapeleka katika wilaya zenye changamoto ya utumishi,” alisema.

Aliitaja mikoa ya changamoto hiyo kuwa ni pamoja na Katavi, Kigoma, Rukwa, Mbeya, Shinyanga, Manyara, Mtwara na Lindi. 

Mulugo alisema licha ya Serikali kupanga kuajiri walimu 28,638 utafiti unaonyesha kuwa walimu wote waliopo katika vyuo vya ualimu, havikidhi idadi ya uhitaji wa Serikali.

Alisema ajira hizo kwa mujibu wa ikama ya Serikali, zitatangazwa rasmi Januari mwakani, huku akiwaonya wahitimu wa shahada ya kwanza ya ualimu katika fani mbalimbali.

Mulugo aliwataka wahitimu hao wasithubutu kupenyeza vijinyaraka kwa wakubwa wizarani, kuomba kuteuliwa kuwa maofisa elimu wa wilaya na mikoa.

Naibu waziri huyo alisema, Serikali imegundua tatizo kuhusu walimu waliotoroka kazini na kujiunga na vyuo vya elimu ya juu pasipo ridhaa ya mwajiri.

Alisema tatizo hilo limeiathiri zaidi mikoa iliyopo Kanda ya Ziwa na mikoa ya Kaskazini, ambayo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu.

“Nawatangazia kiama, wale ambao walitoroka kazini na kuja kujiunga na vyuo vya elimu ya juu pasipo ridhaa ya mwajiri wake…Wizara imewaagiza maofisa elimu wa wilaya na mikoa, kuleta haraka majina hayo wizarani ili tuchukue hatua,” alisema Mulugo.

Mkuu wa chuo hicho, Prof. Amandina Lihamba alisema baadhi ya miradi ya ujenzi wa miundo mbinu imekwama na hivyo kuathiri shughuli za taaluma chuoni hapo.

Alisema ni asilimia 49 ya wanafunzi ndiyo wanaoishi ndani ya chuo na kwamba asilimia 51 iliyosalia wanaishi nje ya chuo, jambo ambalo alisema ni moja ya changamoto kubwa.

Profesa Lihamba alisema, chuo chake kimepokea Sh  bil 1.3 tu kutoka Hazina, zilizoidhinishwa na Serikali na kueleza kuwa, fedha hiyo haitoshi kukamilisha miradi ya chuo hicho.

mtanzania

No comments:

Post a Comment