Changamoto inayotokana na upatikanaji wa mitaji, hasa fedha ya kuendeshea shughuli za kijasiriamali.
Tunapoongelea mtaji tunamaanisha vitu vingi wakiwemo watu, ingawa katikamuktadha huu tuna maanisha fedha ambazo mjasiriamali anahitaji ili aweze kuanzisha na hatimaye kuendesha biashara yake kwa mafanikio.
Katika biashara, mitaji inatokana na vyanzo mbalimbali, chanzo kimojawapo kikiwa ni mkopo kutoka ama kwa mtu binafsi au taasisi za kifedha kwani tunaamini kuwa mjasiriamali yeyote yule kuna wakati huwa anahitaji mkopo.
Kimsingi mikopo imekuwa ni changamoto kubwa katika nchi nyingi zinazoendelea, hasa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kutokana na ukweli kuwa wajasiriamali hawa, wengi wao, wako katika mfumo usio rasmi na hawana anuani maalum za makazi na biashara zao. Vilevile, wajasiriamali wamekuwa wakichukuliwa kama wateja ambao hawawezi kutoa pato kubwa kwa taasisi za kifedha kutokana na hadhi na mazingira ya biashara zao na hivyo kuonekana kama watu wa “mwisho” katika kupewa mkopo.
Pamoja na Serikali kuanzisha mifuko mbalimbali ya kuwasaidia wajasiriamali, mifuko hiyo imekuwa na changamoto mbalimbali kama vile kutotosheleza mahitaji na wakati mwingine kutolewa kwa upendeleo na baadhi ya watendaji wa Serikali wasiowaaminifu.Vilevile taasisi za kifedha zimekuwa zikiwatoza riba kubwa kiasi kwamba marejesho yao yanakomba hata mitaji yao jambo ambalo linawasababishia baadhi yao kufilisika au kushindwa kupiga hatua zaidi.
Pia, taasisi za kifedha zimekuwa zikiwapa kiwango kidogo cha mkopo ambacho hakikidhi mahitaji yao kiasi kwamba baadhi yao huamua kuachana na biashara walizoombea mikopo na kufanya zile ambazo zinaendana na mitaji waliyonayo.
Kwa vile mikopo wanayopewa haikidhi hata nusu ya mahitaji yao ya biashara, baadhi yao hujikuta wakishindwa kutimiza ndoto zao za kufanyabiashara kama walivyopanga na hivyo ama kukimbia kulipa deni au kulipa katika mazingira magumu ambayo huwa katisha tamaa ya kuendelea na biashara baada ya kulipa deni.
Hali kadhalika inaonesha kuwa maafisa mikopo wa taasisi za kifedha wasiowaadilifu wamekuwa ni changamoto kubwa kwa wajasiriamali hawa kwa kuwadai rushwa ya asilimia 10 ya fedha wanayokopa benki kwa madai ya kuwasadia katika kufanikisha kupata mikopo.
Matokeo ya madai ya asilimia 10 kutoka kwa wajasiriamali hawa ni kuwaongezea mzigo wa marejesho, na pale wanaposhindwa wanaamua kukimbiana kuiingiza taasisi husika katika matatizo. Pamoja na wajasiriamali hawa kujaribu mbinu mbadala ya kujiunga katika vikundi ili waweze kupata hata hicho kiasi kidogo kwa ajili ya kuendeshea biashara zao, bado vikundi hivyo navyo vina changamoto zake.
Baadhi ya wanakikundi wasio waaminifu huamua kukimbia na fedha za mkopo na hivyo kuwaachia wenzao mzigo mkubwa ambao licha ya kuwarudisha nyuma kibiashara, huwaletea matatizo katika familia zao hasa pale taasisi hizo zinapoamua kuchukua vitu vya familia kama fidia ya fedha iliyokopwa kutoka katika taasisi husika.
Makala hii itaendelea wiki ijayo Mwandishi ni mtunzi wa vitabu
s:M'nchi
No comments:
Post a Comment