Tafiti zinaonyesha sababu za wanafunzi kutokuwapo shuleni ni pamoja na utoro, mimba za utotoni, umaskini na mwamko mdogo wa wazazi kuhusu elimu.
Wakati ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 , ikionyesha kuwa asilimia 44 ya Watanzania wote ni watoto chini ya umri wa miaka 15, watoto milioni mbili na nusu wamebainika kukosa fursa ya kupata elimu ya msingi.
Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu, anasema kuwa sababu kubwa ya watoto wengi kutokuwapo shuleni licha ya kuwa na umri wa kwenda shule ni utoro.
“Hata ukiangalia BEST (Kitabu cha Takwimu za Elimu ya Msingi) ya mwaka 2012 utaona kuwa utoro ulikuwa sababu kubwa ya watoto kutokuwa shuleni,” anasema.
Anaeleza kuwa, utoro huo unachangiwa na mambo kadhaa, ikiwamo umaskini na baadhi ya wazazi kutokuona umuhimu wa elimu.
Anataja sababu nyingine kuwa ni mimba za utotoni, ambazo hata hivyo anasema zinachangia sehemu ndogo ya watoto kutokuwa shuleni.
Kuhusu watoto wasioandikishwa kabisa shuleni, Bunyazu anasema kuwa hali hiyo inachangiwa na wazazi kutokuona umuhimu wa elimu kwa watoto wao.
Tatizo la dunia
Siyo Tanzania pekee, tatizo la watoto kukosa fursa za elimu linaikabili dunia nzima. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki –Moon, hadi kufikia mwaka 2011, takwimu zinaonyesha watoto milioni 57 hawakuwepo shuleni.
“Watoto milioni 57 hawako shuleni, wanarandaranda mitaani. Kila ninapotembelea nchi kama vile huko Afrika nimeona watoto wanarandaranda mitaani au wanacheza, kwa nini wako hapo?’’ anahoji na kuongeza:
“Wanapaswa wakati huo wawepo shuleni. Hiyo ni dira yetu, lazima wote tuwarudishe shule. Kila siku watoto 19,000 wenye umri chini ya miaka mitano wanakufa kutokana na magonjwa yanayozuilika. Ni lazima tuokoe vifo hivyo vinavyoweza kuepukika.”
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikiri kuwepo kwa changamoto nyingi katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu.
Hata hivyo, anasema kuwa, jukumu la Serikali ni kukabiliana na changamoto hizo, kwani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki kwa kila mwananchi kupatia elimu.
“Sera ya elimu nchini inaonyesha umuhimu wa kuhakikisha elimu inapatikana kwa watu wote na kwa jinsia zote,’’ aliongeza kusema.
Watoto na umaskini
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), linasema kuwa iwapo watoto wote wangepata elimu, mapato ya kila mtu yangeongezeka kwa asilimia 23 katika kipindi cha miaka 40.
“Elimu ina uwezo wa kipekee wa kupunguza umaskini wa kupindukia na kuchagiza malengo ya maendeleo kwa jumla,” inasema ripoti moja ya UNESCO.
Aidha, ripoti hiyo inaongeza kusema kuwa kama wanawake wote wangalipata elimu ya msingi, ndoa za utotoni na vifo vya watoto vingepungua kwa theluthi moja, huku vifo vya kinamama wajawazito vikipungua kwa theluthi mbili.
Ripoti ya Sensa 2012
Ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonyesha watoto wenye umri kuanzia sifuri hadi miaka 14 ni 19,725,456 sawa na asilimia 43.9 ya Watanzania wote.
Kwa kawaida watoto hawa wanapaswa kuwa shuleni. Taarifa kuwa watoto milioni mbili hawako shule zinatia doa jitihada za Serikali katika utekelezaji wa mipango kama vile Elimu kwa Wote, pamoja na kufikia malengo ya Maendeleo ya Milenia
mwnchi
No comments:
Post a Comment