Chumvi imepewa majina mengi kulingana na jamii ambayo mengine yanachekesha
Kila Jumapili ya mwisho ya mwezi Septemba kila mwaka huitwa Siku ya Moyo Duniani.
Lengo la siku hiyo ni kuwapa ufahamu watu kuhusu magonjwa ya moyo ambayo ndiyo kwa kiasi kikubwa husababisha vifo kwa wingi duniani. Tukio hili hulenga pia katika kuhamasisha njia za kujikinga na zinazoweza kusaidia kupunguza hatari ya kupata magonjwa hayo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa mwaka 2005 peke yake palitokea vifo vya watu milioni 17.2 duniani kwa magonjwa ya moyo.
Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2020 magonjwa ya kuambukiza yatakuwa na uwiano sawa na magonjwa yasiyoambukiza, yaani asilimia 50 kwa 50 kwa nchi za Afrika ambako kwa sasa vifo vingi husababishwa na magonjwa ya kuambukizwa kama vile, malaria, kifua kikuu na Ukimwi.
Hii ni kutokana na maendeleo ya kiuchumi ambayo huambatana na magonjwa yasiyoambukiza kama vile, shinikizo la damu, shambulizi la moyo, figo, kiharusi na kisukari. Siku ya magonjwa ya moyo duniani inakwenda sambamba na matumizi ya kiungo muhimu kiletacho ladha katika chakula, yaani chumvi.
Chumvi ni kitu chenye kihistoria duniani, tangu miaka milioni iliyopita chumvi imekuwapo na kutumika duniani.
Chumvi ni moja ya vitu vilivyomo katika maji ya baharini, baada ya maji kuwa mvuke baada ya kupata joto, chumvi hubaki kama vichangarawe vidogovidogo ambavyo huvunwa na kutumika.
Ukipita majumbani, hoteli zote, migahawa, minadani, matamasha na mitaani vijiwe vya nyama choma utashuhudia ulaji mkubwa wa chumvi. Watu hujimiminia chumvi katika chakula hata kama chakula hicho kina chumvi. Wengi wao hawafahamu kama ulaji chumvi kwa mtindo huo ni hatari kwa afya zao.
Tabia za kikemikali za chumvi
Chumvi ni muhimu sana kwa mwili wa mwanadamu kwa kuwa huwa na kiambata kiitwacho sodium ambacho ni muhimu kwa kazi za kimwili. Kikemikali, chumvi imebeba sodium chloride, ndani yake takriban asilimia asilimia 40 kati ya hizo ni sodium.
Mfumo wa fahamu hutumia sodium kwa ajili ya mipitisho mbalimbali, ukunjikaji au kujivuta kwa misuli, udhibiti wa kiwango sahihi cha maji na uwiano sahihi wa chumchumvi mwilini hutegemea sodium.
Sodium huweza pia kuipata katika vyakula mbalimbali, kiambata cha sodium huwa na tabia ya kuvuta maji kwenda mahali ilipo. Mwili hutumia sodium kwa ajili ya kudhibiti wingi wa maji katika damu, ogani na tishu za mwilini.
Pale chumvi inapozidi, basi figo huwa na kazi ya kuitoa kwa njia ya mkojo. Ingawa kama utakula kwa kiasi kingi, basi figo hushindwa kutoa kiasi chote hivyo huendelea kubaki mwilini ndipo matatizo mbalimbali hujitokeza.
Madhara ya chumvi kiafya
Shinikizo la damu
Msukumo wa damu mwilini hutegemea na uwepo wa sodium. Pale sodium inapokuwa imezidi mwilini, msukumo wa damu nao unakuwa juu na hatari. Uwepo zaidi wa sodium ni pale mhusika anapokuwa tayari ana shinikizo la damu, ugonjwa ambao huwa haonyeshi dalili mwanzoni.Mgonjwa hugundulika pale anapokuwa anapata matibabu mengine hospitalini. Kiasi cha damu katika mzunguko ni moja ya vitu vinavyosababisha uwepo wa msukumo wa damu mwilini.
Pale utakapokula kiasi kikubwa cha chumvi zaidi ya uwezo wa figo zako kuhimili kiasi kilichozidi cha chumvi mwilini hubaki, kutokana na tabia ya sodium kuvuta maji kiasi kilichozidi kitabakisha maji mengi mwilini na hivyo ujazo wa damu utaongezeka katika mzunguko na hivyo shinikizo la damu hutokea.
Vilevile, sodium iliyopo kwenye chumvi hutegemewa na seli za misuli ya moyo ili kuongeza mapigo, pale inapozidi mapigo huwa juu na hivyo shinikizo la damu hutokea.
Ndiyo maana huwashauri wagonjwa wenye shinikizo la damu kupunguza chumvi kwenye chakula hasa ya kuongeza. Pia, watu ambao kwao kuna historia ya shinikizo la damu ni vizuri kuchunga na kupunguza matumizi chumvi katika chakula.
Magonjwa mengine ya moyo na kiharusi
Kula chumvi nyingi kunasababisha magonjwa mengine ya moyo na kiharusi (stroke). Kama msukumo wa damu utakuwa mkubwa zaidi inaweza ikasababisha mishipa yako ya damu ikawa inashindwa kutanuka na kukuweka katika hatari ya kujengeka kwa mrundikano wa mafuta kitaalamu huitwa plaque.
Hali inasababisha tatizo katika mishipa ya damu kitaalamu huitwa atherosclerosis.Tatizo hili ni hali ya mishipa kuwa migumu. Mishipa ya ateri huweza kuharibika na kuwa myembamba au kusinyaa na kuta za mishipa hiyo hukakamaa. Hali hii huufanya moyo kuwa na kazi ngumu na hivyo inakuweka katika hatari ya kupata shambulizi la moyo la ghafla, moyo kushindwa kufanya kazi na kusababisha kiharusi.
Tafiti za shule ya afya ya jamii ya Harvard, Marekani inaonyesha utumiaji chumvi kupita kiasi inaongeza asilimia 23 ya kuweza kupata kiharusi na asilimia 14 kupata magonjwa ya moyo.
Matatizo mengine ni kama vile moyo kuwa mkubwa na valvu kuwa na matatizo, kwani uwepo wa ujazo mkubwa katika mzunguko wa damu inamaanisha moyo kufanya kazi ya ziada ili kuleta mzunguko sahihi unaotakiwa na mwili.
Kadiri muda unavyosonga na uwepo wa hali hii husababisha moyo kuongezeka ukubwa na valvu za moyo huwa nyembamba. Hali hii huleta dalili kama vile maumivu ya kifua, kushindwa kupumua na kuwa na mchoko sugu. Pia, kifo cha ghafla na moyo kushindwa kufanya kazi huweza kutokea.
Pia, chumvi husababisha magonjwa mengine kama ya figo, mwili kuvimba na upungufu wa maji, tindikali kuwa nyingi tumboni, udhaifu wa mifupa, vichochezi na chumvi chumvi katika mwili kutowiana.
Nini cha kufanya?
Moja ya nyenzo kuu za kupambana na tatizo hili ni kubadili mienendo na mifumo ya kimaisha kwa kuhakikisha tunaepuka ulaji vyakula wa chumvi kwa kuongeza mezani, kuacha ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, sukari nyingi na vyakula vyenye wanga kupita kiasi. Hakikisha sahani yako ya chakula imesheheni kwa wingi mboga za majani na matunda, kunywa maji mengi, kufanya mazoezi na kupima afya mara kwa mara.
No comments:
Post a Comment